Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu Irenius Ruyobya wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya Mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Oktoba, 2017 ambao umepungua hadi kufikia asilimia 5.1 ikilinganishwa na asilimia 5.3 ilivyokuwa mwezi Septemba, 2017. Kulia Meneja wa Takwimu za Ajira na Bei Bi. Ruth Minja.
Na: Veronica Kazimoto,
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Oktoba, 2017 umepungua hadi kufikia
asilimia 5.1 ikilinganishwa na asilimia 5.3 ilivyokuwa mwezi Septemba, 2017.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa
Shughuli za Kitakwimu Irenius Ruyobya wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)
amesema kupungua kwa Mfumuko wa Bei kunamaanisha kuwa, kasi ya
mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Oktoba, 2017
imepungua ikilinganishwa na kasi ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia Septemba,
2017.
Ruyobya ameongeza kuwa, kupungua kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Oktoba,
2017 kumechangiwa na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula kwa
kipindi kilichoishia mwezi Oktoba, 2017 zikilinganishwa na bei za mwezi
Oktoba, 2016.
"Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa Mfumuko wa Bei ni
pamoja na unga wa mtama kwa asilimia 2.6, samaki kwa asilimia 7.1, matunda
kwa asilimia 2.7, mbogamboga kwa asilimia 7.4, maharage kwa asilimia 2.9,
viazi kwa asilimia 14.4 na karanga kwa asilimia 7.8", amesema Ruyobya.
Akizungumzia Mfumuko wa Bei kwa upande wa Afrika Mashariki, Irenius
Ruyobya amesema Mfumuko wa Bei wa Tanzania una mwelekeo unaofanana
na baadhi ya nchi nyingine za Afrika Mashariki ambapo nchini Kenya
Mfumuko wa Bei wa mwezi Oktoba, 2017 umepungua hadi asilimia 5.72
kutoka asilimia 7.06 mwezi Septemba, 2017 na nchini Uganda umepungua hadi
asilimia 4.8 mwezi Oktoba, 2017 kutoka asilimia 5.3 mwezi Septemba, 2017.
Mfumuko wa Bei wa Taifa unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za
bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
No comments:
Post a Comment