Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Selemani S. Jafo (Mb), ameiagiza Mikoa yote nchini kuanza mapema maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2018, kufuatia kuongezeka kwa ufaulu.
Mhe. Jafo ametoa kauli hiyo mjini Dodoma, wakati akiongea na Waandishi wa Habari, juu ya kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka, 2018,
“Wakuu wa Mikoa hakikisheni miundombinu iliyopo inatosha katika mikoa yenu ili watoto wote waliofaulu, wapate nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza hapo Januari, 2018”, ameitaja mikoa ya Dar es Salaam, Geita, Kagera, Njombe, Tanga, Morogoro, Lindi, Rukwa, Pwani, Mtwara na Songwe kuwa na idadi kubwa zaidi na hivyo maandalizi ya madarasa, vyoo na madawati yatahitajika kwa kiwango kikubwa.
Aidha, amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa, kusimamia zoezi la uchaguzi wa wanafunzi tarajiwa wa kidato cha kwanza ili ifikapo Desemaba 8, 2017 wawe wamekwisha tangaza.
Mhe. Jafo ameagiza kufanyika uchambuzi ili kubaini sababu zilizopelekea watahiniwa zaidi ya asilimia moja kutofanya mitihani katika mikoa ya Geita, Katavi, Mara, Rukwa, Songwe, Dodoma na Manyara kwa lengo la kuondoa mdondoko wa wanafunzi kutoka ngazi moja hadi nyingine.
Pia amezitaka Halmashauri zilizopata ufaulu chini ya asilimia hamsini kujiwekea mikakati ya kupandisha ufaulu wa wanafunzi, Halmashauri hizo ni pamoja na Mkalama, Meatu na Simanjiro.
Matokeo ya darasa la saba, yalitangazwa rasmi hivi karibuni, ambapo jumla ya watahiniwa wapatao 662,035 walifaulu kwa kupata madaraja ya A, B na C, ikiwa ni sawa na asilimia 72.76 ya watahiniwa wote.
Ofisi ya Rais TAMISEMI, yenye dhamana na usimamizi wa Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari imechukua hatua za makusudi, ili kupunguza au kuondoa wanafunzi waliofaulu mtihani wa darasa la saba kutopangiwa shule na kujiunga na kidato cha kwanza mwaka, 2018.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Selemani S. Jafo (Mb), akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu Maagizo aliyoyatoa kwa Mikoa kuwapokea wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka, 2018. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu (ELIMU) Ofisi ya Rais TAMISEMI, Tixon Nzunda na Mkurugenzi Msaidizi (ELIMU SEKONDARI) OR TAMISEMI.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Selemani S. Jafo (Mb), akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu Maagizo aliyoyatoa kwa Mikoa kuwapokea wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka, 2018.
Wanafunzi (watahiniwa) wa shule ya Msingi Miningani, Halmashauri ya Mji, Kondoa, Dodoma wakifanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka, 2017
No comments:
Post a Comment