WANAFUNZI sita wa darasa la kwanza katika shule ya msingi Kihinga wilaya ya Ngara mkoani Kagera wamefariki na wengine 24 kujeruhiwa baada ya kulipukiwa na bomu la mkono jana asubuhi wakati wakiingia darasani.
Akiongea kwa njia ya simu na blog ya jamii Diwani wa
kata ya Kibogora wilayani Ngara Adronis Bulindoli amesema bomu hilo limewalipukia wanafunzi hao kabla ya kuingia darasani na waliojeruhiwa wamekimbizwa hospitali ya Misheni ya Rulenge kwa ajili ya kupewa matibabu
Amesema waliofariki wana umri kati ya miaka 8 hadi 9 na kwamba askari polisi wa kituo kidogo cha Kata ya Bugarama na askari wa jeshi la wananchi kikosi cha kulinda mpaka katika kata ya Bugarama wilayani Ngara wako eneo la tukio wakiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Aidha amesema wanafunzi watatu walifariki papo hapo huku wengine wamepoteza maisha wakiwa wanakimbizwa hospitali ya Rulenge,Jeshi la polisi wanaendekea na uchunguzi wa kubaiini chanzo cha kulipuka bomu hilo.
Naye mwenyekiti wa halmshauri ya wilaya ya Ngara Erick Nkilamachumu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa wauguzi na wafanya kazi wa hospitali ya Rulenge wanafanya juhudi za kuokoa maisha ya wanafunzi waliojeruhiwa katika tukio hilo.
Kata za Bugarama na kibogora ilipo shule ya msingi Kihinga ni mpakani mwa nchi jirani ya Burundi na baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wanadai huenda bomu hilo lililetwa na wanafunzi wanaokuja shuleni kuuza vyuma chakavu.
Aidha Mganga mkuu wa Hospitali ya Misheni Rulenge Mariagoleti Fransis amekiri kupokea wanafunzi 18 majeruhi ambapo wanafunzi wawili walipoteza maisha kabla ya kufikishwa katika hospitali hiyo na walijeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao.
Mkuu wa Wilaya ya Ngara Luteni Kanali Michael Mangwela Mntenjele amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo vya wanafunzi hao.
"Nimepata taarifa na mimi hizo sasa hivi nipo kwenye hii shuhuri ya Rais hapa Kagera sugar nikimaliza naenda Ngara ili kujua zaidi lakini nimeshatuma wataalam wangu wameenda eneo la tukio"alisema.
No comments:
Post a Comment